Makubaliano Ya Leseni Ya Mtumiaji Wa Hatima Wa Programu Ya Showmax

Makubaliano haya ya leseni ya mtumiaji wa mwisho wa programu ya Showmax ("Makubaliano ya Leseni") yanatumika kwa utumiaji wako wa programu ya Showmax. Tafadhali soma vigezo hivi kwa umakini.

1. UTUMIAJI WAKO WA PROGRAMU YA SHOWMAX UNAUNDA MAKUBALIANO

1.1 Showmax ("Showmax" au "sisi" au "nasi" au "yetu") inatoa huduma ya utazamaji wa maudhui popote ulipo ("Huduma ya Showmax") ambayo watumiaji wanaweza kuitumia kutazama au kupakua kwa muda vipindi vya televisheni, filamu, video au klipu za sauti na maudhui mengine kama hayo ya sauti na picha ("Maudhui") kwa kutumia kifaa cha kielektroniki kinachoweza kuunganishwa kwenye intaneti, ikijumuisha kompyuta za watu binafsi, simu za mkononi, tableti, vicheza faili za sauti na video, televisheni inayoweza kuunganishwa kwenye intaneti (Smart TV), ving'amuzi, vifaa vya michezo ya video na vifaa vingine kama hivyo ("Kifaa cha Kufikia").

1.2 Ili watumiaji wafikie na kupokea Huduma ya Showmax kwa kutumia Kifaa cha Kufikia, tumesanidi au tumetoa programu ya Showmax, ambayo pia inajumuisha nyenzo za ufafanuzi zinazohusiana, mwongozo wa maagizo na nyenzo zingine ambazo tunaweza kuamua kutoa pamoja na, au kama sehemu ya programu "Showmax App").

1.3 Tafadhali kumbuka kuwa yafuatayo yamejumuishwa katika Makubaliano ya Leseni na ni sehemu ya Makubaliano ya Leseni:

1.3.1 sera yetu ya faragha ("Sera ya Faragha"); na

1.3.2 vigezo na masharti yetu (“Vigezo na Masharti”).
Tafadhali tembelea tovuti ya Showmax ili upate maelezo zaidi.
Neno lolote linaloanza kwa herufi kubwa ambalo halijafafanuliwa katika Makubaliano haya ya Leseni, litakuwa na maana lililopewa katika Vigezo na Masharti au Sera ya Faragha.

1.4 Kwa kukubali Makubaliano ya Leseni, unakubali pia kufuata masharti ya Sera ya Faragha, kama ambayo yamejumuishwa kikamilifu katika Makubaliano haya ya Leseni.

1.5 Makubaliano haya ya Leseni yanaeleza vigezo na masharti yanayotumika kwa upakuaji, ufikiaji na utumiaji wako wa Programu ya Showmax na yataanza kutumika tarehe ambayo utaanza kupakua au kutumia Programu ya Showmax.

1.6 Wakati mtu ("mtumiaji", "wewe", au "mwenzako") anapakua, anafikia au anatumia Programu ya Showmax, unakubali pia Makubaliano haya ya Leseni. Ikiwa hukubali Makubaliano haya ya Leseni, hupaswi na huruhusiwi kupakua, kufikia au kutumia Programu ya Showmax.

1.7 Hatukuuzii Programu ya Showmax chini ya Makubaliano haya ya Leseni, na tunabaki kuwa wamiliki wa Programu ya Showmax wakati wote.

2. JINSI YA KUFIKIA NA KUPAKUA PROGRAMU YA SHOWMAX

2.1 Vifaa

2.1.1 Ili upakue na kufikia Programu ya Showmax lazima uwe na Kifaa cha Kufikia.

2.1.2 Kifaa cha Kufikia lazima kitimize vipimo vya kiufundi vya kwiango cha chini kama inavyoelezwa kwenye Tovuti ya Showmax mara kwa mara.

2.1.3 Vifaa Fulani vya Kufikia na mifumo ya uendeshaji huenda visifanye kazi na Programu ya Showmax kutokana na masharti au vizuizi vinavyohusiana na Kifaa cha Kufikia au mfumo wa uendeshaji. Hatutawajibika kwa hali yako ya kutoweza kupakua au kufikia Programu ya Showmax kutokana na vizuizi vinavyohusiana na Kifaa chako cha Kufikia.

2.1.4 Wewe kwa gharama yako binafsi, unawajibika kwa kununua na kutunza Vifaa, kupata muunganisho thabiti na wa kutegemewa wa intaneti kutoka kwa mtoa huduma unayependelea na watoa huduma wa mawasiliano ya simu, huduma, bidhaa na vifaa vingine vyote vinavyohitajika kufikia intaneti au kupakua Programu ya Showmax (“Teknolojia”).

2.1.5 Ikiwa Kifaa cha Kufikia si chako, unathibitisha kuwa umepata ruhusa kutoka kwa mwenye Kifaa cha Kufikia ya kupakua au kuweka Programu ya Showmax kwenye Kifaa husika cha Kufikia na kutumia Programu ya Showmax kulingana na vigezo vya Leseni hii ya Mtumiaji.

2.1.6 Hatuwajibiki kwa gharama zozote za kufikia huduma ya intaneti, gharama za mtoa huduma na gharama za utumiaji wa data. Ni lazima wewe au mwenye Kifaa cha Kufikia alipie gharama hizi.

2.1.7 Iwapo utatatizika na Teknolojia unayotumia kufikia na kutumia Programu ya Showmax, ni wajibu wako kuwasiliana na, na kujaribu kutatua matatizo hayo na watoa huduma wako binafsi wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT) na mawasiliano ya simu na watoa huduma, kabla ya kuwasiliana nasi ili tukusaidie.

2.1.8 Unathibitisha na kukubali hatari kuwa maelezo yanayotumwa kupitia intaneti au mfumo mwingine wa mawasiliano, ikiwa ni pamoja mfumo wa mawasiliano usiotumia muunganisho wa waya, yanaweza kufikia, kutekwa, kubadilishwa na kufuatiliwa bila idhini na kinyume cha sheria.

2.2 Ni lazima upakue Programu ya Showmax
2.2.1 You Ni lazima upakue Programu ya Showmax kwenye Kifaa cha Kufikia kutoka kwenye duka la programu (App Store) linalohusiana na Kifaa cha Kufikia.

3. UTOAJI NA UPEO WA LESENI YA KUTUMIA PROGRAMU YA SHOWMAX

3.1 Leseni

3.1.1 Iwapo utafuata masharti ya Mkataba huu wa Leseni, tunakupa leseni binafsi, isiyoweza kuhamishwa, isiyo ya kipekee, isiyoweza kutoa leseni ndogo na inayoweza kufutwa, ya kupakua, kusakinisha na kutumia App ya Showmax kwenye Vifaa vya Ufikiaji kwa madhumuni ya kibinafsi pekee na sio ya kibiashara.

3.1.2 Hatukupatii haki au leseni zozote za kufikia au kutumia msimbo wa chanzo wa Programu ya Showmax.

3.2 Leseni na Masharti ya Utumiaji

3.2.1 Tunaweza kutoa maagizo, ilani, miongozo na maelekezo mara kwa mara kuhusiana na matumizi, utekelezaji, utendakazi na usalama wa Programu ya Showmax. Ni lazima utii maagizo, ilani, miongozo na maelekezo haya.

3.2.2 Ni lazima utufahamishe mara moja ikiwa utashuku au utagundua tukio lolote halisi, linalodhaniwa au linaloshukiwa la utumiaji wa Programu ya Showmax bila idhini.

3.2.3 Isipokuwa kama inavyoelezwa wazi katika Leseni hii ya Makubaliano au kama inavyoruhusiwa na sheria, hupaswi:

3.2.3.1 kutoa leseni ndogo, kuuza, kupangisha, kukodisha, kuhamisha (ikiwa ni pamoja na kupitia uhamishaji wa kifaa au mali zingine), kukabidhi, kutumia kwa makusudi ya ofisi ya huduma au kuruhusu ufikiaji kwa muda, kusambaza upya au kutoa Programu ya Showmax au sehemu yake yoyote kama dhamana;

3.2.3.2 kunakili, kubadilisha au kubuni miigo ya Programu ya Showmax, isipokuwa iwapo hatua hiyo ya kunakili inaambatana na utumiaji wa kawaida wa Programu ya Showmax, au kuunganisha Programu ya Showmax na programu au zana zingine;

3.2.3.3 Kutumia App ya Showmax kwa namna yoyote, ikiwemo kufanya mabadiliko, nakala, kuunganisha, kutafsiri, au kufanya uhandisi wa kinyume wa App ya Showmax au sehemu yoyote yake, ikijumuisha kwa uwazi lebo za HTML, msimbo wa JavaScript, msimbo wa kitu, programu-jalizi, au msimbo mwingine wowote unaotumika kuruhusu matumizi ya App ya Showmax, kwa lengo la kuunda, kusaidia, kuboresha au kuruhusu matumizi, au vinginevyo kukuza bidhaa au huduma nyingine, ikiwemo bidhaa au huduma za ushindani.

3.2.3.4 kubomoa, kutenganisha, kukwepa teknolojia yoyote ya kuficha msimbo, kufanya utafiti wa kihandisi au kujaribu kugundua msimbo wa chanzo, msimbo wa kijenzi au muundo wa msingi, mawazo, ujuzi au algoriti zinazohusiana na Programu ya Showmax au sehemu yake yoyote;

3.2.3.5 kujihusisha katika, kuendeleza au kuhimiza shughuli haramu kwa kutumia Programu ya Showmax;

3.2.3.6 kufanya kitendo chochote cha kinyume cha sheria, cha uvamizi, cha kuingilia, cha kudhalilisha au cha udanganyifu kwa kutumia Programu ya Showmax au sehemu yake yoyote, au kutumia Programu ya Showmax kwa njia ambayo inadhuru, ya udanganyifu, ya ulaghai, ya kutishia, ya kunyanyasa, ya kudhalilisha, ya lugha chafu au vinginevyo isiyoruhusiwa au ya kinyume cha Leseni hii ya Makubaliano;

3.2.3.7 kusambaza, kuweka au kuruhusu kuwekwa kwa Msimbo wowote Hasidi kimakusudi au bila kujali kwenye, au kwa kutumia Programu ya Showmax au Teknolojia yake. Msimbo Hasidi ni pamoja na virusi, vidudu, "trojan horses", faili zilizo na virusi, programu hasidi, misimbo danganyifu, maagizo, vifaa au vitu vingine vilivyobuniwa kuharibu, kuvuruga, kutowezesha, kudanganya, kudhuru au vinginevyo kuzuia utumiaji wa Kifaa cha Kufikia, Teknolojia, huduma, data, kifaa cha hifadhi, programu, kifaa au mawasiliano, au vinginevyo kuathiri utendakazi wake.

3.2.3.8 kutoa, kusambaza, kuchapisha au kuwezesha utumaji wa barua pepe zisizohitajika kwa watu wengi, ofa, matangazo au maombi mengine (taka) kwenye au kwa kutumia Programu ya Showmax au kutumia Programu ya Showmax kwa namna ambayo inatekeleza aina yoyote ya jibu la kiotomatiki au taka;

3.2.3.9 kutumia Programu ya Showmax kwa njia inayoathiri utendakazi unaofaa wa Programu ya Showmax (ikiwa ni pamoja na kuweka mzigo mkubwa kwenye Mfumo);

3.2.3.10 kubadilisha, kuficha au kufuta taarifa zozote za haki za uvumbuzi, ikiwa ni pamoja na katika au kwenye sehemu yoyote ya Programu ya Showmax;

3.2.3.11 kuathiri au kuvuruga kimakusudi au bila kujali uadilifu au utendakazi wa Programu ya Showmax au data yoyote iliyomo;

3.2.3.12 kujaribu kufikia bila idhini sehemu yoyote ya Programu ya Showmax au kukiuka au kukwepa kifaa au mbinu yoyote ya usalama iliyojumuishwa katika Programu ya Showmax;

3.2.3.13 kufichua kwa mshirika mwingine yeyote au kuruhusu mshirika mwingine yeyote kufikia sehemu yoyote ya Programu ya Showmax, isipokuwa kama inavyoruhusiwa moja kwa moja katika Leseni hii ya Makubaliano;

3.2.3.14 kujaribu kutumia mfumo wa uendeshaji wa msingi wa Programu ya Showmax;;

3.2.3.15 kutumia Programu ya Showmax kufanya uamuzi kumhusu mtu binafsi kulingana tu na uchakataji wa kiotomatiki unaosababisha athari za kisheria kwa mtu huyo au vilevile ulio na athari kubwa kwa mtu huyo, ikijumuisha, kwa mfano, kubainisha iwapo mtu anastahili kupokea mkopo, bima au kuajiriwa;

3.2.3.16 kutumia Programu ya Showmax, kwa shughuli zozote zenye hatari kubwa, ambapo utumiaji au kutoweza kutumia Programu ya Showmax kunaweza kusababisha kifo, jeraha kwa mtu binafsi au uharibifu wa mazingira;

3.2.3.17 kukusanya au kutafuta maelezo au data yoyote ya kujaribu kutambua jinsi data inavyotumwa kutoka kwenye seva au mifumo inayoendesha Programu ya Showmax;
("Masharti ya Leseni").

3.3 Ukibadilisha au ukijaribu kubadilisha Kifaa chako cha Kufikia kwa njia yoyote au kutumia programu iliyobuniwa kubadilisha Kifaa chako cha Kufikia, kubatilisha au kuzima vipengele vyovyote vya usalama kwenye Kifaa chako cha Kufikia au mfumo wake wa uendeshaji, unathibitisha kuwa unafanya hivyo kwa tahadhari yako binafsi. Kuna vipengele vya usalama vilivyojumuishwa katika Programu ya Showmax ambavyo vimebuniwa kufanya kazi na Kifaa cha Kufikia kulingana na vipimo vya mtengenezaji. Kubadilisha Kifaa cha Kufikia au mfumo wake wa uendeshaji kunaweza pia kusababisha Programu ya Showmax isifanye kazi kabisa.

3.4 Ni lazima uhakikishe kuwa kila mtu anayeweza kutumia Kifaa chako cha Kufikia au Teknolojia nyingine yoyote kwenye kifaa ambako umeweka, umepakua au unatumia Programu ya Showmax, anatii Masharti ya Leseni.

3.5 Unapaswa kutii sheria au kanuni zote za uuzaji au udhibiti wa teknolojia zinazotumika kwa Teknolojia inayotumika au inayofanya kazi na Programu ya Showmax.

3.6 Vitendo au usahaulifu wote wa mtu yeyote anayetumia Kifaa chako cha Kufikia au kifaa kingine chochote ambako Programu ya Showmax imewekwa au inatumika, vitazingatiwa kuwa, na pia vitachukuliwa kuwa ni vitendo na usahaulifu wako. Tunaweza kukuwajibisha kwa vitendo na usahaulifu huu.

4. MABADILIKO KATIKA MAKUBALIANO YA LESENI NA PROGRAMU YA SHOWMAX

4.1 Mabadiliko katika Makubaliano ya Leseni

4.1.1 Tunaweza kubadilisha Makubaliano haya ya Leseni wakati wowote na tutakufahamisha kuhusu mabadiliko hayo. Tutafanya hivyo kwa kukutumia barua pepe au kupitia taarifa ibukizi unapofikia Huduma ya Showmax au Tovuti ya Showmax, au kupitia taarifa ibukizi unapoingia katika akaunti tutakayokufungulia baada ya kujisajili ili kutumia Huduma ya Showmax ("Akaunti ya Showmax"), au kupitia Programu ya Showmax..

4.1.2 Ikiwa hukubali mabadiliko yaliyofanywa katika Makubaliano haya ya Leseni, unaweza kukomesha utumiaji wako wa Programu ya Showmax kwa njia iliyoelezwa katika kifungu cha 6 hapa chini.

4.2 Mabadiliko katika Programu ya Showmax

4.2.1 Tunaweza kusasisha Programu ya Showmax mara kwa mara na tuna haki ya kufanya mabadiliko mara kwa mara katika jinsi tunavyotoa na kuendesha Programu ya Showmax App.

4.2.2 Tunaweza kwa hiari yetu mara kwa mara kubadilisha, kutofautisha au kurekebisha muundo, mwonekano, utendakazi na maudhui ya Programu ya Showmax, ikiwa ni pamoja na kupitia Masasisho na Uboreshaji.

4.2.3 Tunaweza kufanya Masasisho na Maboresho katika Programu ya Showmax mara kwa mara bila kukutoza. Utatakiwa kupakua na kuweka kwenye kifaa Masasisho na Maboresho hayo kutoka kwenye maduka husika ya programu (App Store) ya Vifaa vya Kufikia ili uendelee kutumia Programu ya Showmax.

4.2.4 Kulingana na hali ya Sasisho au Boresho, huenda usiweze kutumia Programu ya Showmax hadi utakapopakua toleo jipya kabisa la Programu ya Showmax.

4.2.5 Si lazima tukufahamishe kuhusu mabadiliko, Masasisho na Maboresho hayo isipokuwa iwapo yataathiri vibaya zaidi uwezo wako wa kutumia Programu ya Showmax, ambapo tutakufahamisha kuhusu mabadiliko hayo angalau siku 10 kabla ya mabadiliko hayo kuanza kutumika.

4.2.6 Ikiwa hukubali mabadiliko yaliyofanywa katika Programu ya Showmax, unaweza kukomesha utumiaji wako wa Programu ya Showmax kwa njia iliyoelezwa katika kifungu cha 6..

4.2.7 Makubaliano haya ya Leseni, kama tunavyoweza kuyarekebisha, yatatumika katika Masasisho na Maboresho yote, isipokuwa tueleze vinginevyo.

5. TUNAWEZA KUSIMAMISHA PROGRAMU YA SHOWMAX NA UTUMIAJI WAKO WA PROGRAMU YA SHOWMAX

5.1 Kuongezea kwa haki na suluhu zingine zozote tunazoweza kuwa nazo katika Makubaliano haya ya Leseni, Vigezo vya Showmax au katika sheria, tuna haki (lazima hatulazimishwi) ya kusimamisha kwa muda sehemu au Programu yote ya Showmax au kusimamisha au kukomesha haki yako ya kufikia na kutumia Programu ya Showmax pale ambapo:

5.1.1 tunahitaji kufanya matengenezo, Maboresho au Masasisho katika Programu ya Showmax au katika mifumo, programu, Teknolojia au miundo mbinu yoyote tunayotumia kutoa Programu ya Showmax au huduma za Showmax;

5.1.2 Showmax ina sababu za kutosha kuamini kuwa unatumia Programu ya Showmax kiholela, bila kujali zaidi au kwa nia ya kufanya ulaghai au kwa makusudi ya udanganyifu;

5.1.3 Showmax ina sababu za kutosha kuamini kuwa unajihusisha katika shughuli yoyote halisi au inayoshukiwa au inayodhaniwa ya ukiukaji wa Masharti ya Leseni;

5.1.4 Showmax itatambua shughuli yoyote halisi, inayodhaniwa au inayoshukiwa ya utumiaji wa Programu ya Showmax bila idhini;

5.1.5 Showmax ina sababu za kutosha kuamini kuwa usalama au Mfumo wa Vifaa vyako vya Kufikia unaotumika kuendesha Programu ya Showmax huenda umeathiriwa;

5.1.6 Showmax itatambua kuwa maelezo yoyote uliyotupatia ni ya uongo, si sahihi, hayatumiki, si kamili au yanapotosha;

5.1.7 ni lazima tufanye hivyo ili kutii sheria; au

5.1.8 tukitakiwa tufanye hivyo na mahakama au mdhibiti.

5.2 Tutaendelea kusimamisha huduma kwa muda ambao tunaamini kuwa unafaa.

5.3 Tutakufahamisha ikiwa tutasimamisha sehemu au Programu yote ya Showmax au utumiaji wako wa Programu ya Showmax ambapo ni wazi kuwa inafaa kufanya hivyo.

5.4 Bila kuathiri haki na suluhu zetu zingine tulizo nazo katika Makubaliano haya ya Leseni, Vigezo vya Showmax au katika sheria, tukitekeleza haki zetu za kusimamisha huduma zilizo katika aya hii ya 5, tutarejesha uwezo wa kufikia na kutumia Programu ya Showmax haraka iwezekanavyo tutakaporidhika kuwa sababu ya kusimamishwa imeondolea, imeepukwa au imeshughulikiwa kabisa.

6. KUKOMESHA MAKUBALIANO YA LESENI

6.1 Jinsi unavyoweza kukomesha Makubaliano haya ya Leseni

6.1.1 Unaweza kukomesha Makubaliano haya ya Leseni wakati wowote bila sababu kwa kufuta kabisa, kuondoa na kuharibu nakala zote za Programu ya Showmax ulizohifadhi au unazodhibiti na ambazo umeweka kwenye Vifaa vya Kufikia.

6.2 Jinsi tunavyoweza kukomesha Makubaliano haya ya Leseni kwa kutoa taarifa

6.2.1 Tuna haki wakati wowote na kwa sababu yoyote ya kukomesha:

6.2.1.1 Makubaliano haya ya Leseni;

6.2.1.2 utumikaji au upatikanaji wa Programu ya Showmax; au

6.2.1.3 haki yako ya kutumia Programu ya Showmax.

6.2.2 Tunapofanya mambo hayo, tutakupa taarifa ya mapema ya maandishi siku 10 kabla isipokuwa:

6.2.2.1 ukomeshaji huo unatakiwa kisheria; au

6.2.2.2 inafaa kupeana kipindi cha chini ya siku 10, kulingana na sababu za kuchukua hatua hizi.

6.3 Athari za kukomeshwa

6.3.1 Makubaliano haya ya Leseni yakikomeshwa kwa saabbu yoyote:

6.3.1.1 haki na leseni zote ulizopewa chini ya Makubaliano haya ya Leseni zitakoma mara moja;

6.3.1.2 unapaswa kukomesha mara moja shughuli zote zilizoidhinishwa na Makubaliano haya ya Leseni;

6.3.1.3 lazima uondoe na kufuta mara moja Programu ya Showmax kwenye Vifaa vyote vya Kufikia na uharibu mara moja nakala zote za Programu ya Showmax unazomiliki, ulizohifadhi au unazodhibiti na (tukiomba) ututhibitishie kuwa umefanya hivyo; na

6.3.1.4 unakubali kuwa tunaweza kufikia kwa mbali Vifaa vya Kufikia na kuondoa na kufuta Programu ya Showmax na nakala zake zote.

6.4 Vigezo ambavyo vitaendelea kutumika

6.4.1 Masharti mengi ya Makubaliano haya ya Leseni yataendelea kutumika baada ya Makubaliano haya ya Leseni kukomeshwa, ikiwa ni pamoja na vigezo na masharti ambayo kwa jinsi yalivyo lazima yaendelee kutumika. Hii ni kwa sababu haki na wajibu fulani lazima uendelee kutumika hata kama makubaliano kati yetu yamekomeshwa au umeacha kutumia Programu ya Showmax.

6.4.2 Baadhi ya masharti yaliyo kwenye Makubaliano haya ya Leseni yatakayoendelea kutumika ni pamoja na (lakini si tu):

6.4.2.1 vigezo na masharti ambapo dhima na wajibu wetu hauzingatiwi au umedhibitiwa, ikiwa ni pamoja na kiasi cha pesa unachoweza kudai kutoka kwetu;

6.4.2.2 vigezo na masharti ambapo haki ulizo nazo dhidi yetu zimedhibitiwa au hazizingatiwi;

6.4.2.3 vigezo na masharti ambapo unawajibika kwa hasara au uharibifu fulani unaoweza kutokea;

6.4.2.4 kifungu cha 8 kinachohusiana na Sera ya Faragha; na

6.4.2.5 kifungu cha ufafanuzi wa Makubaliano haya ya Leseni.

7. MALI YA UVUMBUZI

7.1 Katika Makubaliano haya ya Leseni, "Haki za Mali ya Uvumbuzi" inajumuisha haki za mali ya uvumbuzi za namna na hali yoyote popote duniani, ikiwa ni pamoja na (lakini si tu) hakimiliki na haki husika, hataza, haki za hataza, miundo, haki za miundo, haki za uvumbuzi, haki za hifadhidata, ujuzi, maelezo ya siri, siri za biashara, chapa za biashara, majina ya biashara, majina ya vikoa na alama za huduma, nia njema na haki zingine zote za mali ya uvumbuzi, iwe zimesajiliwa au hazijasajiliwa, ambazo zitaendelea kutumika au zitaendelea kutumika kwa sasa au baadaye katika sehemu yoyote duniani, na ikiwa ni pamoja na haki zote za kudai fidia ya uharibifu wa mali kutokana na ukiukaji, uingiliaji au matumizi mabaya ya haki hizo zozote za mali ya uvumbuzi.

7.2 Unathibitisha kuwa:

7.2.1 haki, sehemu, umiliki na maslahi yote, ikiwa ni pamoja na Haki za Mali ya Uvumbuzi, vilivyo katika na kwenye Programu ya Showmax, Teknolojia na Maudhui vinavyotumika na/au kuonyeshwa kuhusiana na Programu ya Showmax na/au Huduma za Showmax vinamilikiwa na au tumepewa leseni yake na vinalindwa na sheria na vinabaki kuwa mali yetu kamili na ya watoa leseni wetu; na

7.2.2 umepewa leseni (hujauziwa) ya utumiaji wa Programu ya Showmax, na kuwa huna haki, sehemu, umiliki au maslahi yoyote, ikiwa ni pamoja na Haki zozote za Mali ya Uvumbuzi katika, au kwenye Programu ya Showmax, Teknolojia au Maudhui kuliko haki ya kutumia Programu ya Showmax kulingana na vigezo vya Makubaliano haya ya Leseni.

7.3 Huna haki ya kufikia Programu ya Showmax katika muundo wa msimbo wa chanzo.

7.4 Hupaswi kutumia Programu ya Showmax kwa njia yoyote ambayo inasababisha ukiukaji wa sheria yoyote (ikiwa ni pamoja na sheria ya mali ya uvumbuzi), au uingiliaji wa haki zetu (ikiwa ni pamoja na Haki za Mali ya Uvumbuzi), au haki za watoa leseni wetu au mshirika mwingine yeyote.

7.5 Nakala zozote za Programu ya Showmax unazoruhusiwa kutoa kulingana na Makubaliano haya ya Leseni lazima ziwe na hakimiliki sawa na taarifa zingine za uvumbuzi zilizo kwenye Programu ya Showmax.

8. UKUSANYAJI WA DATA

8.1 Sera ya Faragha

8.1.1 Tunakusanya na kuchakata maelezo yako binafsi unapopakua na kuweka kwenye kifaa Programu ya Showmax na kujisajili na kutumia Huduma ya Showmax. Tutasimamia shughuli ya ukusanyaji, uchakataji na uhifadhi wa maelezo yako binafsi kulingana na Sera yetu ya Faragha.

8.1.2 Masharti ya Sera yetu ya Faragha yamejumuishwa kama marejeleo katika Makubaliano haya ya Leseni, na ukikubali vigezo vya Makubaliano haya ya Leseni, unakubali pia kufuata masharti ya Sera ya Faragha, kama ambayo masharti yake yamejumuishwa kikamilifu katika Makubaliano haya ya Leseni.

8.2 Data ya kiufundi na mahali

8.2.1 Kwa kutumia Programu ya Showmax au Huduma zozote za Showmax, unatupatia idhini ya kukusanya na kutumia maelezo ya kiufundi kuhusu Vifaa vya Kufikia na Teknolojia, programu, maunzi na vifaa husika vya kuunganishwa. Tutatumia maelezo haya kuboresha bidhaa zetu na kutoa Huduma zozote za Showmax.

8.2.2 Programu ya Showmax itatuwezesha kutumia data ya mahali inayotumwa kwetu kutoka kwenye Vifaa vya Kufikia. Unaweza kuzima kipengele hiki wakati wowote kwa kuzima mipangilio ya huduma za kufikia data ya mahali katika Programu ya Showmax kwenye Kifaa cha Kufikia. Ukitumia Programu ya Showmax, unatupatia idhini sisi na washirika wetu na watoa leseni, kutuma, kukusanya, kuhifadhi, kuchakata na kutumia data yako ya mahali na maswali ili kutoa na kuboresha bidhaa na huduma zinazolingana na mahali. Unaweza kuondoa idhini hii wakati wowote kwa kuzima mipangilio ya huduma za mahali katika Kifaa chako cha Kufikia.

8.3 Tovuti za washirika wengine
Programu ya Showmax inaweza kuwa na viungo vya tovuti za washirika wengine wanaojitegemea ("Tovuti za Washirika Wengine"). Hatuna uwezo wa kudhibiti Tovuti za Washirika Wengine, na hatuwajibiki na hatuidhinishi maudhui au sera zao za faragha. Utahitaji kutumia busara yako mwenyewe kuhusu utumiaji wako wa Tovuti za Washirika Wengine, ikiwa ni pamoja na ununuzi na utumiaji wa bidhaa au huduma zozote zinazopatikana kupitia tovuti hizo.

9. MAKANUSHO, KUKANWA KWA MAHAKIKISHO, UKOMO WA DHIMA NA FIDIA

9.1 Kanusho na kukanwa kwa mahakikisho

9.1.1 Kadri inavyoruhusiwa na sheria, Programu ya Showmax inatolewa kwa msingi wa "kama ilivyo" na "kama inavyopatikana" na bila hakikisho au dhamana yoyote, iwe ya moja kwa moja, ya kudhaniwa au ya kisheria (ikiwa ni pamoja na mahakikisho yoyote yanayodhaniwa ya kutegemewa, kufaa kwa kusudi lolote maalum au kutokuwa na hitilafu au kasoro).

9.1.2 Kadri inavyoruhusiwa na sheria, hatutoi mahakikisho na hatutoi dhamana kuhusu (i) utumiaji, ubora, uoanifu, upatikanaji au utendakazi wa Programu ya Showmax, au (ii) kuwa Programu ya Showmax:

9.1.2.1 itapatikana au kufikiwa kila wakati;

9.1.2.2 huduma yake haitakatizwa, itapatikana kwa wakati, haitakuwa na hitilafu, itakuwa salama au haitakuwa na Msimbo Hasidi; au

9.1.2.3 itatimiza mahitaji yako binafsi.

9.1.3 Kadri inavyoruhusiwa na sheria, unawajibika kibnafsi kwa hatari za uwekaji kwenye kifaa, utumiaji na matokeo unayopata kwenye Programu ya Showmax.

9.2 Vikomo vya dhima yetu

9.2.1 A Kadri inavyoruhusiwa na sheria, hatutawajibika kwako (na tunakanusha dhima yote) kwa hasara, dhima, jeraha au uharibifu wowote wa mali (uwe wa moja kwa moja, usio wa moja kwa moja, maalum, wa adhabu au unaoambatana) wa namna yoyote kutokana na:

9.2.1.1 hali yoyote ya kukatizwa au kuacha kutumwa kwa maudhui kwenye au kutoka katika Programu ya Showmax au Teknolojia tunayotumia kutoa au kupokea Huduma ya Showmax au Maudhui;

9.2.1.2 Msimbo wowote Hasidi unaoweza kutumwa kwenye au kupitia Programu ya Showmax, Tovuti ya Showmax, Huduma ya Showmax au Maudhui;

9.2.1.3 kasoro, hitilafu au hali yoyote ya kuacha kufanya na/au kucheleweshwa katika Kifaa chako, au Mfumo, maunzi na/au programu;

9.2.1.4 kasoro, hitilafu na/au hali yoyote ya kucheleweshwa kuunganishwa kwenye intaneti;

9.2.1.5 kupotea kwa data yoyote kutokana na uwekaji kwenye kifaa au utumiaji wa Programu ya Showmax;

9.2.1.6 ufikiaji au utumiaji wowote wa Mfumo wetu ambao haujaidhinishwa na/au maelezo yoyote na yote ya binafsi yaliyohifadhiwa humo iwe ni kulingana na dhamana, mkataba, ukiukaji au nadharia nyingine yoyote ya kisheria, na iwapo tumefahamishwa au hatujafahamishwa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa hasara, dhima, jeraha au uharibifu huo.

9.2.2 Masharti ya kifungu cha 9.2 yanatumika bila kujali iwapo dai lolote ambalo wewe au wengine wanawasilisha, au hasara, dhima, jeraha au uharibifu uliopata, unalingana na dhamana, mkataba, ukiukaji au nadharia nyingine yoyote ya kisheria, na iwapo tumefahamishwa au hatujafahamishwa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa uharibifu huo.

9.3 Fidia

9.3.1 Kadri inavyoruhusiwa na sheria, unatulipa fidia na unakubali kutotuwajibisha sisi, washirika wetu na watoa huduma wetu kutokana na hasara, dhima, gharama na uharibifu wowote ambao sisi au wao wanaweza kupata kutokana na dai, ambapo dai hilo linatokana na:

9.3.1.1 wewe kuingilia au kutumia vibaya haki za mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na Haki za Mali ya Uvumbuzi;

9.3.1.2 wewe kukiuka Masharti yoyote ya Leseni na Utumiaji; na

9.3.1.3 kitendo chochote cha kimakusudi au cha kinyume cha sheria unachofanya au kutochukua hatua.

10. TAARIFA

10.1 Anwani ambazo tunakubali zitumike kutuma taarifa, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria
Taarifa zozote tunazotumiwa chini ya Makubaliano haya ya Leseni, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria, lazima ziwasilishwe kwetu ana kwa ana au kupitia posta katika ofisi za Showmax zilizoko (i) 144 Bram Fischer Drive, Randburg, Johannesburg, Gauteng, 2194, Afrika Kusini; au (ii) Plot 1381 Tiamiyu Savage Street, Victoria Island, Lagos, Naijeria; au (iii) 27 Old Gloucester Street, London, Uingereza, WC1N 3AX, Uingereza; au (iii) kupitia barua pepe katika help@showmax.com
Taarifa zozote tunazokutumia chini ya Makubaliano haya ya leseni, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria, zitatumwa kwenye anwani uliyoweka ulipokuwa unapakua Programu ya Showmax au anwani nyingine yoyote uliyotufahamisha ipasavyo, au kwenye anwani yako ya barua pepe ikiwa uliiweka kama njia unayopendelea ulipokuwa unapakua Programu ya Showmax.
Hata hivyo, taarifa zozote tunazoweza kukutumia na uzipokee kuhusiana na makubaliano mengine yoyote tuliyoweka nawe au kwa njia zingine, itazingatiwa kuwa taarifa ya kutosha.
Iwapo utabadilisha anwani zako na ukose kutufahamisha kwa kusasisha maelezo yako kwenye Tovuti ya Showmax, unakubali kuwa utakubali kupokea taarifa, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria, kwenye anwani uliyoweka ulipokuwa unapakuwa Programu ya Showmax.
Pia, tuna haki ya kukutumia taarifa kupitia SMS au barua pepe, au unapoingia katika Akaunti ya Showmax, au kwenye Tovuti ya Showmax, au kupitia Programu ya Showmax, tukiwa tunakusudia kusimamisha au kukomesha Makubaliano haya ya Leseni au utumiaji wako wa Programu ya Showmax, au tukiwa tumebadilisha sehemu yoyote ya Makubaliano ya Leseni, au tunapofanya mabadiliko, Masasisho au Maboresho katika Programu ya Showmax.
Hupaswi kujiondoa ili usipokee taarifa kutoka kwetu kuhusu maelezo hayo ya hapo juu.

10.2 Anwani ambazo unakubali zitumike kukutumia taarifa, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria

10.2.1 Iwapo ulichagua barua pepe kama njia ya mawasiliano unayopendelea ukiwa unajisajili, unakubali kuwa tunaweza kutuma taarifa, ikiwa ni pamoja na taarifa za kisheria kwenye anwani yako ya barua pepe.

10.3 Taarifa zinazotumwa kupitia SMS au barua pepe kupitia Programu ya Showmax

10.3.1 Tuna haki ya kukutumia taarifa kuhusu masuala yafuatayo kupitia SMS au barua pepe au kupitia Programu ya Showmax:

10.3.1.1 taarifa kuwa tunakusudia kusimamisha au kukomesha Makubaliano haya ya Leseni au utumiaji wako wa Programu ya Showmax; na

10.3.1.2 taarifa kuwa tumerekebisha au kusasisha sehemu yoyote ya Makubaliano ya Leseni.

10.3.2 Hupaswi kujiondoa ili usipokee taarifa kutoka kwetu kuhusu maelezo ya hapo juu.

10.4 Matangazo ya moja kwa moja

10.4.1 Tunaweza kukutumia taarifa mara kwa mara kuhusu matangazo ya ofa, majarida au mapendekezo au maelezo ambayo tunaweza kufikiri kuwa yanaweza kukufaa au kukuvutia.

10.4.2 Unaweza kujiondoa wakati wowote ili usipokee mawasiliano haya, kwa kufuata kiungo cha jiondoe kilicho kwenye mawasiliano.

10.4.3 Unaweza pia kuwasiliana nasi kupitia maelezo yaliyotolewa katika aya ya 11 ili upate usaidia wa kujiondoa ili usipokee mawasiliano ya matangazo ya moja kwa moja.

11. USAIDIZI NA MALALAMIKO

11.1 Iwapo utapata matatizo yoyote ya kiufundi kuhusiana na sehemu yoyote ya Programu ya Showmax, au iwapo unataka kuwasilisha malalamiko, unaweza kuwasiliana na timu yetu ya usaidizi wa kiufundi kupitia barua pepe katika help@showmax.com.

12. MASUALA YA ZIADA

12.1 Hupaswi kuhamisha au kukabidhi Makubaliano haya ya Leseni na haki, wajibu na leseni zozote zinazotolewa chini yake.

12.2 Tunaweza wakati wowote kuhamisha, kupeana au kukabidhi haki na wajibu wowote au wote chini ya Makubaliano haya ya Leseni. Tutakufahamisha iwapo tutahamisha, kupeana au kukabidhi haki au wajibu wowote kwa mshirika mwingine. Si lazima tukufahamishe tunapokabidhi haki au wajibu wowote kwa washirika au wakandarasi wetu wowote wadogo tunaoweza kuwateua.

12.3 Makubaliano haya ya Leseni yatatumika kwa manufaa ya, na yatafuatwa kisheria na warithi na wawakilishi wa kila mshirika.

12.4 Makubaliano haya ya Leseni na uhusiano kati ya Mteja wa Afrika Kusini nasi, yatasimamiwa na sheria za Jamhuri za Afrika Kusini.

12.5 Makubaliano haya ya Leseni na uhusiano kati ya Mteja wa nje ya Jamhuri ya Afrika Kusini nasi, yatasimamiwa na sheria za Uingereza na Wales.

12.6 Hatua yetu ya kutoweza kutumia au kutekeleza haki au sharti lolote la Makubaliano haya haipaswi kuchukuliwa kuwa tumeachilia haki au sharti hilo. Ikiwa sharti lolote la Makubaliano haya litabainishwa kuwa si sahihi na mahakama inayotambulika (ikiwa ni pamoja na, lakini si tu, kwa sababu sharti hilo halilingani na sheria za eneo lingine) au halitumiki, pande husika hata hivyo zinakubali kuwa mahakama inapaswa kujitahidi kutekeleza nia za pande husika jinsi inavyobainishwa katika sharti hilo.

12.7 Makubaliano haya ya Leseni yanaunda makubaliano yote kati yako nasi kuhusiana na leseni ya Programu ya Showmax. Kadri inavyoruhusiwa na sheria, hakuna yeyote kati yako nasi anayelazimishwa kutii sharti, sheria, kiapo, hakikisho au ahadi yoyote kuhusiana na Programu ya Showmax ambayo haijaandikwa katika Makubaliano haya.

12.8 Makubaliano haya ya Leseni yanaweza kutolewa katika lugha kadhaa. Iwapo kutakuwa na tofauti zozote, toleo la Kiingereza linatumika.

12.9 Kila sharti la Makubaliano haya ya Leseni, na kila sehemu ya sharti lolote, inaweza kuondolewa na kutenganishwa na sehemu zingine. Kadri inavyoruhusiwa na sheria, ikwia sharti lolote la Makubaliano haya, au sehemu ya sharti haitaweza kutekelezwa, itakuwa kinyume cha sheria au si sahihi, lazima ichukuliwe kana kama haikujumuishwa katika Makubaliano haya. Masharti yaliyosalia ya Makubaliano haya bado yataendelea kutumika na kutekelezwa.

12.10 Katika Makubaliano haya ya Leseni, vichwa vimewekwa ili kurahisisha mambo wala si kutumika katika kufafanua vigezo hivi, na isipokuwa ielezwe wazi vinginevyo au vinginevyo ihitajike kulingana na muktadha:

12.10.1 marejeleo ya umoja yanajumuisha wingi na kinyume chake;

12.10.2 maneno yaliyo katika jinsia fulani yanajumuisha jinsia zingine (mwanamume, mwanamke na jinsi isiyoegemea upande wowote). Marejeleo ya jinsia isiyoegemea upande wowote (kwa mfano 'wao' au 'hicho') inajumuisha jinsia zote;

12.10.3 maneno au vifungu ambavyo vimefafanuliwa au kuandikwa kwa herufi kubwa katika Vigezo hivi, vitakuwa na maana sawa vinapotumika katika Vigezo hivi;

12.10.4 neno ‘ikiwa ni pamoja na’ au 'inajumuisha' au ' pamoja na' halipaswi kuchukuliwa kuwa linatumika tu kwa orodha inayofuata neno hilo au haijumuishi vitu vingine kwenye orodha inayofuata neno hilo. Neno:

12.10.4.1 'ikiwa ni pamoja na' inamaanisha 'ikiwa ni pamoja na, lakini si tu';

12.10.4.2 'inajumuisha' inamaanisha 'ni pamoja na, lakini si tu'; na

12.10.4.3 'pamoja na' inamaanisha 'pamoja na, lakini si tu'; na

12.10.5 iwapo idadi yoyote ya siku imetolewa, siku hizo zinahesabiwa bila kujumuisha siku ya kwanza lakini zinajumuisha siku ya mwisho.

12.11 Tuna haki ya kusasisha Makubaliano haya ya Leseni (1) iwapo masharti mapya yatasasishwa na washirika wetu; au (2) iwapo tutafanya mabadiliko katika huduma na bidhaa zetu.